Wenye Thamani Kuliko Tuwazavyo: Watu Machoni pa Mungu | Lesson 3 || 12/01/2025
Вставка
- Опубліковано 14 січ 2025
- Kama tulivyoona katika somo lililotangulia, hakuna mtu -hata mwenye dhambi mbaya kabisa au mwovu kuliko wote-ambaye Mungu hampendi. Na kwa sababu Mungu anawathamini watu zaidi ya vile tunavyoweza kufikiria, anachukizwa na dhambi kwa sababu anatupenda na anajua dhambi inachotufanyia, pia.
Soma Luka 15:11-32. Mfano wa mwana mpotevu unafunua nini kuhusu huruma na upendo wa Mungu? Unatoa onyo gani kwa wale ambao, kama yule mwana mwingine, walibaki nyumbani?
Katika kisa hiki anachosimulia Yesu, mwana wa mtu huyo aliomba urithi wake mapema, akimkataa baba yake na nyumba ya baba yake kabisa. Kisha mwana mpotevu anakwenda na kutapanya urithi wake na anafikia hali ya umaskini na njaa, akitamani chakula wanachokula nguruwe katika kihori. Akitambua kwamba watumishi katika nyumba ya baba yake wana chakula cha kutosha, anaamua kurudi nyumbani kwa matumaini ya kuwa mtumishi.
Kinachofuata kina nguvu. Akina baba wengine wangemfukuza mtoto kama huyo anaporudi. “Ulichukua urithi wako na kujiondoa nyumbani kwangu. Huna nyumba tena hapa.” Huo ungekuwa mtazamo wenye mantiki, na wenye maana kabisa, sivyo? Machoni pa baadhi ya wazazi wa kibinadamu, mwana huyo alikuwa ameenda mbali sana kiasi cha kutowezekana kurejeshwa nyumbani tena, hasa kama mwana.
Lakini, katika mfano huo, baba (anayemwakilisha Mungu Mwenyewe) haitikii kwa njia mojawapo ya hizi. Badala yake, “ ‘[mwana mpotevu] alipokuwa angali mbali, baba yake alimwona, akamwonea huruma, akaenda mbio akamwangukia shingoni, akambusu sana' ” (Lk. 15:20). Ijapokuwa nyakati kama hizo ilionekana kuwa jambo lisilo la heshima kwa bwana mwenye nyumba kukimbia kwenda kumlaki mtu fulani, baba huyo kwa huruma yake kubwa alikwenda mbio kumlaki mwanawe na, cha kushangaza zaidi, akamrudisha nyumbani mwake, hata kumfanyia sherehe, ikionesha huruma kubwa ya Mungu kwa kila mtu mpotovu na furaha anayokuwa nayo hata mtu mmoja kurudi nyumbani. Ni taswira ya Mungu ya kuvutia kiasi gani!
Kinachouvutia ni mwitikio wa mwana mwingine. Kwa nini mwitikio huu ulikuwa mwitikio wa kibinadamu, ulioegemezwa angalau kwa sehemu juu ya haki, na unaoeleweka sana, vilevile? Hata hivyo, sehemu yake ya kisa inatufundisha nini kuhusu jinsi dhana za kibinadamu za haki hazifikii kina cha injili au upendo wa Mungu kwetu?
Amina