KATIBU MKUU WIZARA YA AFYA APONGEZA UJENZI WA HOSPITALI CHUO CHA UFUNDI ARUSHA (ATC)
Вставка
- Опубліковано 24 лис 2024
- Kufuatia uhitaji mkubwa wa wataalamu wa matengenezo ya vifaa tiba nchini Chuo cha Ufundi Arusha kinajenga hospitali ambayo Pamoja na huduma za afya na za kisasa zitakazotolewa kwa jamii yote, pia itasaidia kutoa mafunzo kwa wanafunzi wanaosoma program ya Uhandisi umeme na Vifaa Tiba.
Akizungumza wakati alipotembelea Chuoni hapo kukagua ujenzi wa hospitali hiyo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Dkt. John Jingu amekipongeza Chuo cha Ufundi Arusha kwa kuamua kujenga hospitali hiyo na kusema kwamba Wizara ya Afya itatoa ushirikiano wa namna hospitali hiyo itakavyofanya kazi.
“Nawapongeza kama Chuo kwa uamuzi wenu mzuri wa kujenga hospitali hii, eneo hili la uhandisi wa vifaa tiba ni muhimu sana, Wizara ya Afya inatumia fedha nyingi sana kununua vifaa hivi lakini baada ya kununuliwa kazi kubwa ipo kwenye kuvitunza na kuvifanyia matengenezo ili viendelee kufanya kazi kwa sababu hatuna wataalamu wa ndani” alisema Dkt. Jingu.
Aidha Dkt. Jingu aliongeza kuwa “sisi kama Wizara ya Afya tutakua tayari kuwasaidia kwenye eneo hili la mafunzo ili tuweze kupata wataalamu watakaokua wanafanya marekebisho ya vifaa hivi pale inapohitajika”.
Vilevile Dkt. Jingu ameushauri uongozi wa Chuo cha Ufundi Arusha kuwa baada ya hospitali hiyo kukamilika wajitahidi kutoa huduma bora ambazo zitawavutia watu hasa kutoka nchi Jirani za Kenya na Uganda kufuatia ongezeko la watu wengi kufanya utalii wa kutafuta matibabu bora katika nchi mbalimbali.
Kwa upande wake Mkuu wa Chuo hicho Prof. Musa Chacha amesema hospitali hiyo inajengwa kwa mapato ya fedha za ndani na itakapokamilika itasaidia kutoa matibabu kwa wanafunzi na jamii kwa ujumla.
“Tunatumia mapato yetu ya ndani kujenga hospitali hii, matarajio yetu ni kutoa huduma bora kwa wanafunzi wetu na jamii kwa ujumla, lakini kubwa zaidi ni kuwawezesha vijana wetu wanaosoma programu ya Uhandisi Umeme na Vifaa Tiba kufanya mafunzo ya vitendo ili waweze kuwa bora zaidi kwenye eneo la urekebishaji wa vifaa tiba” alisema Dkt. Chacha.