HOTUBA YA RAIS DKT.JOHN MAGUFULI AKIWA ZIARA WIALAYA YA MEATU-SIMIYU

Поділитися
Вставка
  • Опубліковано 21 вер 2024
  • Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli amewaagiza viongozi wa Mikoa na Wilaya zote nchini kwa kushirikiana na Wizara ya Mifugo na Uvuvi kuandaa mipango bora itakayowawezesha wafugaji kufuga mifugo yao bila kuwaathiri wakulima, badala ya kuwafukuza wafugaji katika maeneo yao kwa madai kuwa ni wavamizi.
    Mhe. Rais Magufuli ametoa agizo hilo leo wakati akizungumza na wananchi wa Itilima na Meatu katika ziara yake inayoendelea hapa Mkoani Simiyu.
    Amefafanua kuwa Watanzania wote wana haki ya kuishi mahali popote katika nchi yao hivyo ni wajibu wa viongozi wa Mikoa na Wilaya kutengeneza mipango itakayoainisha maeneo ya malisho na huduma nyingine za mifugo badala ya kufukuza wafugaji kana kwamba sio raia wa Tanzania.
    “Wafugaji na wakulima wanahitajiana, wakulima wanawahitaji ng’ombe na wafugaji wanahitaji mazao ya kilimo, kwa hiyo changamoto ni kwenu viongozi wa Mikoa na Wilaya kutengeneza mipango mizuri itayowapa haki makundi yote kuishi bila migogoro” amesema Mhe. Rais Magufuli.
    Aidha, Mhe. Rais Magufuli ameiagiza Wizara ya Maliasili na Utalii kusimamia vizuri maliasili za Taifa ikiwemo kuzuia uvamizi katika hifadhi za taifa, mapori ya akiba na misitu ya Serikali, pamoja na kuhakikisha wawekezaji na wafanyabiashara wote wanaokuja kuendesha shughuli zao hapa nchini katika sekta ya utalii, wanalipa kodi na tozo zote wanazopaswa kulipa.
    Katika ziara ya leo Mhe. Rais Magufuli ambaye ameongozana na baadhi ya Mawaziri amejibu kero za wananchi kuhusiana na maji, huduma za afya na barabara, ambapo Waziri wa Maji na Umwagiliaji Prof. Makame Mbarawa amemhakikishia Mbunge wa Itilima Mhe. Njalu Silanga na wananchi wake kuwa Serikali inachimba visima 40 vya maji kwa gharama ya Shilingi Bilioni 1.55 na mabwawa 2 yatakayogharimu shilingi Bilioni 1.5 kwa ajili ya vijiji vya Nhobora, Sawira na Mwamapalala, na kwa Mji wa Mwanhuzi ambao ni Makao Makuu ya Wilaya ya Meatu, Serikali imetenga shilingi Milioni 318 kwa ajili ya kuchimba visima 8 vya maji na shilingi Milioni 214 kwa ajili ya kuimarisha mfumo wa usambazaji maji katika Mji huo.
    Nae Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu amesema mwaka huu Serikali imetenga shilingi Milioni 600 kwa ajili ya ujenzi wa zahanati na kituo cha afya katika Jimbo la Itilima, na kwa Wilaya ya Meatu pamoja na kutoa shilingi Milioni 607 kwa ajili ya kuboresha huduma za afya, Serikali ipo katika mipango ya ujenzi wa kiwanda kikubwa cha kuzalisha bidhaa za hospitali kitakachogharimu shilingi Bilioni 29.3.
    Kwa upande wake Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mhe. Selemani Jafo amesema pamoja na kujenga majengo ya Halmashauri ya Itilima katika mwaka huu wa fedha Serikali imetenga shilingi Bilioni 1.5 za kujengea Hospitali ya Wilaya na kwa Jimbo la Kisesa ameahidi kutafuta fedha kwa ajili ya kujenga kituo cha afya.
    Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Isack Kamwelwe amewahakikishia wananchi wa Itilima, Kisesa na Meatu kuwa Serikali itaendelea kuimarisha miundombinu ya barabara na madaraja na kwamba sasa inajiandaa kufanya usanifu wa awali kwa barabara ya Bariadi - Itilima - Kisesa - Mwandoya - Ngoboko ili baadaye ijengwe kwa kiwango cha lami.
    Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mhe. Kangi Lugola amesema kama ambavyo Wizara yake kupitia Jeshi la Polisi imefanya juhudi kubwa kukabiliana na mauaji ya vikongwe na wenye ualbino, inaendelea kufanya juhudi kama hizo kuhakikisha ujambazi, uporaji, wizi na unyanyasaji wa raia na mali zao haupati nafasi, na ametoa wito kwa wananchi kutoa taarifa kila wanapobaini vitendo vya uvunjaji wa sheria.
    Naibu Mawaziri wa Madini Mhe. Doto Biteko na Mhe. Stanslaus Nyongo wameahidi kuendelea kusimamia vizuri rasilimali ya madini na kwamba ili kuvutia uwekezaji zaidi katika uzalishaji wa chumvi tayari Serikali imefuta kodi 8 kati ya 11 zilizokuwepo.
    Katika mkutano wa hadhara uliofanyika Mwanhuzi, Mhe. Rais Magufuli amepokea ombi la Mbunge wa Jimbo la Meatu Mhe. Salum Hamis Salum “Mbuzi” la kujengewa barabara za Mji huo na ameiagiza Wizara ya Ujenzi kuanza ujenzi wa kilometa 3 za barabara hizo ndani ya miezi miwili kuanzia sasa.
    Mhe. Rais Magufuli amemshukuru Mwakilishi Mkazi wa Shirika la umoja wa Mataifa la Idadi ya Watu (UNFPA) Bi. Jacqueline Mahon kwa ufadhili wa shilingi Bilioni 9 za kutekeleza mradi wa Nilinde Nikulinde ambao unaimarisha huduma za afya kwa kupanua zahanati 31, hospitali 2, vituo vya afya 5, kujenga benki ya damu ya Mkoa, kununua magari 9 na kununua vifaa vya hospitali.
    Pia Mhe. Rais Magufuli amefungua majengo ya uboreshaji wa utoaji wa huduma za afya katika Hospitali ya Wilaya ya Meatu kwa niaba ya vituo vingine 39 vya kutolea huduma za afya katika Mkoa wa Simiyu na kuzungumza na wafanyakazi wa hosptali hiyo.

КОМЕНТАРІ • 3

  • @erasmusshauritanga4444
    @erasmusshauritanga4444 6 років тому

    Asante Sana Rais wetu we really like to hear your voice hakika tunafurahi unavyosikiliza kero za wananchi na unavyotoa suluhu.
    May GOD bless you so much.

  • @athumanomary1438
    @athumanomary1438 6 років тому

    Ewe mwenyez MUNGU ewe mwenyez MUNGU tunazidi kukuomba enderea kumuongoza kumsimamia kumrinda na kuimarisha afya yake raisi wetu

  • @alexrija2972
    @alexrija2972 6 років тому

    jpm myama mkari